Kingunge aitaka CCM Impigie Magoti Lowassa kama inataka Kushinda, amwita Magufuli Mteule wa Kufinyangwa


KingungeMWANASIASA mkongwe nchini, Kingunge Ngombale-Mwiru amekitaka Chama cha Mapinduzi (CCM) kumpigia magoti Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, kama kinataka kushinda Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari vya ndani na nje nyumbani kwake, Kijitonyama, Dar es Salaam, Julai 15, 2015, Kingunge alisema Lowassa anashikilia mtaji mkubwa wa mamilioni ya wapigakura, hivyo kama CCM haitampigia magoti na kumuomba ushiriki wake katika kampeni za chama hicho, hakitashinda uchaguzi huo.
Lowassa alikuwa miongoni mwa makada 38 wa CCM waliojitokeza kuchukua na kurejesha fomu za kuomba kuteuliwa na chama hicho katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Hata hivyo, katika mchakato huo wa uteuzi wa CCM, jina la Lowassa lilishindwa kuchomoza hata katika tano bora za Kamati Kuu, hali iliyozua sintofahamu miongoni mwa wajumbe wa vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu.
Majina matano yaliyoibuka katika kikao cha Kamati Kuu yalikuwa ya Bernard Membe, January Makamba, Balozi Amina Salim Ally, Dk Asha-Rose Migiro na Dk John Magufuli, kabla ya majina mawili ya Membe kuishia ndani ya NEC, na hatimaye Mkutano Mkuu wa CCM kumchagua Magufuli kwa kura 2,104, sawa na asilimia 87.1, hivyo kuwaacha nyuma Dk Migiro na Balozi Amina.
"Hadithi ya Lowassa kuwa ni fisadi haina mashiko, ilianza kwa kashfa ya Richmond. Kamati Teule ya Bunge iliundwa na kutoa taarifa za ovyo sana, hatimaye kwa sababu ya kulinda heshima ya Serikali na Chama, akalazimika kujiuzulu,” anasema Kingunge.
Anaongeza: "Lowassa alijiuzulu kwa kuwajibika kisiasa, lakini ikabadilishwa ili aonekane ni yeye aliyefanya makosa…hapo ndipo
ukaanza wimbo wa ufisadi. Serikali yenyewe ilimsafisha kupitia Takukuru, lakini wimbo wa ufisadi ukaendelea, wakaja na wimbo mwingine wa Gamba.”
Akielezea taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ya kwamba Waziri Mkuu huyo wa zamani aliyejiuzulu mwaka 2008 kutokana na kashfa ya kampuni tata ya kufua umeme wa dharura ya Richmond, anataka kuihama CCM na kwenda upinzani, Kingunge alisema kwa hana taarifa hiyo.
“Kilichotokea Dodoma si halali na si haki,” alisema Kingunge na kuongeza: “Lakini CCM lazima iendelee. Tumepata mgombea, John
Magufuli. Yeye si ndo aliyefinyangwa na Wajumbe wa Mkutano Mkuu? Tumuunge mkono.”
Kingunge ambaye msimamo wake unajulikana kuwa alikuwa akimuunga mkono Lowassa katika mbio zake hizo za kusaka urais, alisema hakubaliani na kauli ya Katibu wa NEC (Itikadi na Uenezi), Nape Nnauye, ya kwamba wagombea wasioridhika na uamuzi wa Kamati Kuu hawawezi kukata rufaa kwa sababu ya muda, huku akitoa mfano wa John Malecela aliyekata rufaa na kusikilizwa na NEC mwaka 2005 baada ya kija lake kukatwa na Kamati Kuu.
Katika mitandao mbalimbali ya kijamii nchini, ukiwemo mtandao maarufu wa JamiiForums, kumekuwepo na mjadala mzito kuhusiana na kauli hiyo ya Kingunge ya kutaka CCM impigie magoti Lowassa, vinginevyo chama hicho hakitashinda uchaguzi ujao.

No comments:

Post a Comment