Lembeli katika mahojiano na waandishi wa habari |
Wabunge wawili waliohama CCM hivi karibuni, James Lembeli na
Ester Bulaya wamepitishwa katika kura za maoni kuwania ubunge kupitia
chama chao kipya.
Wakati Lembeli akipitishwa kwa kura
za kishindo kuwania ubunge katika Jimbo la Kahama Mjini, Bulaya
alishinda katika nafasi ya viti maalumu baada ya kushindwa katika
kinyang’anyiro cha Jimbo la Bunda Mjini.
Wanasiasa hao sasa wanasubiri uteuzi wa Kamati Kuu ya Chadema utakaofanyika Agosti 5 na 6.
Ushindi wa Lembeli
Katika
uchaguzi huo wa juzi, mbunge huyo wa zamani wa Kahama aliwabwaga
wenzake 13 aliogombea nao akipata kura 168 kati ya 262 zilizopigwa,
akifuatiwa na John Katibu aliyepata kura 45, Peter Shita (17) na
Emmanuel Madoshi aliyepata kura 10.
Wengine ni Muta
Nyerere (4), Felician Maige (4), Zacharia Obadia (3), Tadeo Mwati (2),
Arnold Mtajwaka (2), Prosper Denga (2), Deusdedit Madinda (1), Reuben
Macheyeki (1). Victor Mbwana na Richard Makingi waliambulia patupu.
Katika uchaguzi wa viti maalumu, Winfrida Mwinula alishinda kwa kura 34
akifuatiwa na Salome Makamba aliyepata kura 30.
Bulaya
Kama
isingekuwa ni kura za maoni za viti maalumu zilizomfuta machozi, Bulaya
alikuwa tayari ametupwa nje baada ya kuanguka katika Jimbo la Bunda
Mjini.
Bulaya aliyekuwa miongoni mwa makada saba wa
chama hicho waliokuwa wanawania kuliwakilisha jimbo hilo, alipata kura
37 kati ya 182 zilizopigwa akiwa nyuma ya Pius Masururi aliyeibuka
mshindi kwa kura 65 na Magembe Makoye aliyepata kura 40.
Baadaye
katika mkutano wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), uliofanyika
baadaye usiku, Bulaya alipata kura 71 kati ya 110 zilizopigwa na
kuwabwaga Godliver Masamaki aliyepata kura 31, Joyce Sokombi (4), Minza
Shani (3), Dk Jane Nyamsenda (1) na Alice Wandya aliyeambulia patupu.
Awali,
Bulaya alikwaa kisiki baada ya jina lake kuwa miongoni mwa waliokatwa
na kamati ya utendaji inayosimamia majimbo hayo wakidaiwa ni wageni
katika chama; wapenda fujo na matabaka, akiwa pamoja na Chacha
Nyamhanga, Sulemani Daudi lakini walirudishwa kundini baada ya kikao cha
viongozi na watiania.
Katika Jimbo la Bunda Vijijini,
Sulemani Daudi aliibuka mshindi kwa kura 84 kati ya 127 zilizopigwana
kuwashinda John Masenza aliyepata kura 14, Dk Lucas Webiro (11), Frank
Mongateko (8), Edgar Chibura (5) na Mathias Bandio aliyepata kura moja.
No comments:
Post a Comment