MAGAZETI LEO ..............


MTANZANIA

Shirika la Umeme Tanzania TANESCO,  limesema haliwezi kutaja bei rasmi ya gharama za umeme wa gesi hadi mtambo utakapoanza kufanya kazi ili kubaini halisi.
Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO  Felchesmi Mramba alisema Tanzania ni nchi ambayo inatumia kiwango cha chini cha gharama za umeme ikilinganishwa nan chi jirani za Afrika Mashariki.
Alisema mitambo ya umeme wa mafuta inatarajia kuzima ifikapo Septemba ndio maana wamesaini mkataba wa miezi mitatu kwa vile mwezi huo ndio mradi wa umeme wa gesi unakamilika.
Alisema mitambo ambayo haitakatishwa mikataba ni ule wa IPTL na Nyakato.
“Mkataba wa shirika la umeme IPTL  ni wa muda mrefu hivyo hatuwezi kukatisha mkataba isipokuwa  tutaiomba ibadilishe mfumo na kutumia gesi  lakini wa Nyakato ni kwa kwetu” Mramba.
Alisema Serikali pia inafanya juhudi za kupunguza utegemezi wa mitambo ya kufua umeme wa  na kutumia mafuta ambayo ni ghali zaidi na kuamua kutekeleza mradi wa Kinyerezi wenye uwezo wa kuzalisha MW 150 ambao utagharimu zaidi ya bilioni 293 na utakamilika Agosti mwaka huu.

NIPASHE

Mchakato wa kumpata mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) umeendelea kuibua mapya na kuleta mvutano baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Prof. Mark Mwandosya, kunukuliwa akisema kuwa majina matano yaliyopelekwa kwenye Kamati Kuu ya CCM (CC) kutoka kwenye Kamati ya Maadili yalijulikana hata kabla ya kikao cha Kamati ya Maadili hakijaketi.
Prof. Mwandosya ambaye ni Mbunge wa Rungwe Mashariki amenukuliwa akisema hayo kwenye sauti yenye maelezo yake iliyorekodiwa na kusambazwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii.
Prof. Mwandosya alisema amepata taarifa za kusambazwa kwa sauti hiyo lakini hafahamu kama yanayozungumzwa humo ni ya kwake.
Prof. Mwandosya alisema anachokumbuka akiwa kijijini kwao Lufilio wilayani Rungwe aliitwa na wazee na kufanya nao mkutano wa ndani wakitaka kujua nini kilichojiri wakati wa mchakato wa kumpata mgombea urais CCM.
“Niliitwa na wazee kwenye mkutano wa ndani wakitaka kujua nini kimetokea na inawezekana yaliyomo ndani ya hiyo clip yana ukweli, lakini wewe unadhani nilichokisema ni uongo?, Si kinalingana na hali halisi ilivyokuwa Dodoma,” alisema.
Hata hivyo, alisema taarifa zilizosambazwa kwamba anataka kuhamia Chadema siyo za kweli.
Katika sauti iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, Prof. Mwandosya amenukuliwa akisema kuwa majina ya makada walioingia tano bora katika kinyang’anyiro cha urais yaliyopelekwa Kamati Kuu yalijulikana hata kabla ya kikao cha Kamati ya Maadili hakijaketi.
Alisema Mwenyekiti wa Kamati Kuu, Rais Jakaya Kikwete, alikuwa na majina yake matano mfukoni na kamati yenyewe pia ilikuwa na majina yake.
Akizungumzia madai hayo, Prof. Mwandosya alithibitisha kuwa madai hayo ni ya kweli na kwamba wajumbe wote wa Mkutano Mkuu wa CCM waliokuwapo Dodoma wanalijua hilo.
“Hapo mimi sioni kwamba kuna jambo ambalo limepotoshwa, kwani yote yanayosemwa ni ya kweli na hata wajumbe wote waliokuwa Dodoma kwenye Mkutano Mkuu wanayajua vizuri mambo hayo,” Prof. Mwandosya.
Alisema ingawa hajaisikia sauti inayodaiwa kuwa ni yake, lakini  kama ni suala la kusema kuwa mgombea urais mteule wa CCM, Dk. John Magufuli hajawahi kuwa hata mwenyekiti wa tawi la CCM ni kweli.
Alizidi kueleza kuwa, anaona ni sahihi kwa sababu katika kumbukumbu zake hajawahi kusikia wala kumwona Dk. Magufuli akiwa Mwenyekiti wa Chama katika ngazi yoyote.
Nina kazi nyingi sijafungua mitandao ya kijamii kwa muda mrefu kidogo, lakini kama mambo yanayosemwa ni hayo, sioni kama kuna uongo ndani yake, ningepata shida sana kama mambo yanayozungumziwa yangekuwa siyo ya kweli, katika kumbukumbu zangu sijawahi kusikia Dk. Magufuli amekuwa Mwenyekiti wa Chama au Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama, lakini sasa ndiye atakayekuwa mwenyekiti wa Chama chetu nadhani hilo liko wazi,” alisema.
Akizungumzia uamuzi wa Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, kuhamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Prof. Mwandosya alisema kuwa Lowassa ametumia haki yake ya kidemokrasia na yeye haoni kama kwa uamuzi huo amefanya kosa lolote.
Alisema vyama vya siasa ni sawa na madhehebu ya dini, ambapo waumini wanayo haki ya kwenda kuabudu katika kanisa wanalolitaka au ambalo imani yao inawatuma na hakuna mtu wa kuwapokonya haki hiyo.
“Alichokiamua Lowassa sidhani kama ana kosa, kwani anayo haki na uhuru wa kufanya alichokifanya, siku hizi kuna makanisa mengi, mtu anapoamua kwenda kuabudu katika kanisa analoona linamfaa huwezi kusema kuwa amekosea, labda ninachoweza kushauri ni CCM kujiuliza sababu za Lowassa kuondoka na ikiwezekana ijisahihishe ili watu wengi zaidi wasiondoke,” alisema.

NIPASHE

Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Job Ndugai amehojiwa na Jeshi la Polisi mkoani Dodoma kwa tuhuma za kumshambulia kwa fimbo na kumjeruhi mgombea mwenzake katika mbio za kuwania ubunge wa Jimbo la Kongwa kwa tiketi ya CCM, Dk. Joseph Chilongani.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, David Misime, alisema kuwa walilazimika kumhoji Ndugai baada ya kupokea malalamiko kuhusiana na tukio hilo lililotokea wilayani Kongwa juzi.
Inadaiwa kuwa Ndugai alimpiga fimbo na kumjeruhi vibaya Chilongani wakati wagombea hao na wenzao watano wanaowania kuteuliwa kuwa wagombea wa ubunge kwa tiketi ya CCM walipokuwa wakijinadi ili wapitishwe na wanachama wenzao jimboni humo.
“Tulipokea malalamiko, tumemhoji Ndugai na kisha tukamuachia kwa dhamana… hivi sasa tunaendelea na uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo,” alisema Kamanda Misime na kuongeza kuwa watatoa taarifa zaidi pindi uchunguzi ukikamilika.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Ezekiel Mpuya, alithibitisha vilevile kuwa Dk. Chilongani alipokewa kwao juzi jioni kwenye Hospitali ya Wilaya ya Kongwa na kwamba hadi kufikia jana alikuwa bado akiendelea na matibatu.
“Anaendelea na matibabu lakini hali yake inaendelea vizuri,” Dk. Mpuya.
 Dk. Chilongani, alisema kuwa juzi, wagombea wote saba walifanya kampeni katika kata tatu na kabla hawajamalizia ngwe hiyo, ndipo sakata hilo lilipozuka.
Aliongeza kuwa wakati wakimalizia kujinadi kwenye kata ya Ugogoni, yeye alipanda jukwaani kujinadi kabla ya kufuatiwa na Ndugai, kwa mujibu wa ratiba waliyopangiwa na kiongozi wa msafara huo.
Alisema Ndugai baada ya kupanda jukwaani, licha ya kunadi sera, alianza kumshambulia (Ngatunga), kwa maneno makali akimtuhumu kuwa amekuwa akishirikiana na watendaji wa halmashauri ya wilaya kufanya ubadhirifu.
Aliposhuka jukwaani, akaendelea kunishambulia kwa maneno, nikamwambia kwa hadhi yako haustahili kufanya siasa za namna hii; akatishia kunipiga,Ngatunga.
Alisema Ndugai kwa kutumia fimbo kubwa aliyokuwa nayo mkononi muda wote, alimpiga Ngatunga kwenye paji la uso na sehemu nyingine za mwili hadi akazimia.

NIPASHE

Baadhi ya makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliomuunga mkono Waziri Mkuu msfaaru, Edward Lowassa, katika mbio zake za kuomba uteuzi wa kugombea urais kabla ya kukihama chama hicho, wamefunguka.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mara, Christopher Sanya, amesema kitendo cha Lowassa, kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kinaashiria chama hicho kumomonyoka, baada ya kumalizika kwa kura za maoni.
Alisema ni pigo kubwa kwa CCM na litasababisha madhara makubwa baada ya kura za maoni kumalizika.
Lowassa ametumia haki yake kufanya hivyo, kama mwenyewe  alivyosema hakuridhishwa na mchakato mzima wa kumpata mgombea urais wa CCM ingawa ni pigo kubwa kwa chama chetu,” alisema Sanya na kuongeza kuwa uamuzi wake sio wa kubeza kwani yeye ni mtu kukatwa  Dodoma alikaa kimya muda mrefu bila kuzungumza chochote hadi alipofikia kuchukua maamuzi hayo ya juzi.
Mbunge wa Mwibara anayemaliza muda wake, Kangi Lugola, alisema uamuzi huo una madhara makubwa kwa CCM hasa kipindi hiki.
“Kwanza namtakia kila la heri katika kuendeleza safari yake ya matumaini, huyu ni mtu mzima, mwenye elimu, amekuwa kiongozi mwandamizi serikalini na mkongwe wa siasa, hivyo hadi kufikia hatua hiyo hakufanya maamuzi ya pupa bali ametumia busara na hekima kubwa,”  Lugola.
Hata hivyo, alipoulizwa endapo atamuunga mkono kwa kuhamia Chadema, alisema anatambua kufanyiwa mizengwe mingi na viongozi wa CCM ngazi ya wilaya, lakini kwa sasa anashiriki katika kura za maoni akiamini viongozi hawawezi kumzuia kuingia bungeni kwa mara nyingine.
“Nilienda Dodoma miaka mitano hii tunayomaliza kwa kupelekwa na wananchi wa Mwibara, wananchi hao hao bado wapo hivyo viongozi wa CCM watambue pia nitapelekwa Bungeni na wananchi hao hao si viongozi wa chama,” Lugola.
 Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga, Hamisi Mgeja, alisema licha ya Lowassa kuwekeza jasho lake kwa kipindi kirefu ndani ya CCM, lakini ana haki na ni mtu mzima ambaye hawezi kuingiliwa katika kufikiwa maamuzi yake.
“Ingawa hili ni jambo kubwa na zito, lakini tumekuwa naye kwa kazi, tumeshirikiana naye kukijenga chama chetu, lakini ikifika mahali huwezi kuzuia mtu kufanya maamuzi yake,” Mgeja.
Hata hivyo, alisema licha ya rafiki yake kuondoka, yeye atabaki kuwa mwana-CCM mwaminifu na muadilifu na mwenyekiti wa mkoa huo.
Mwanasiasa Mkongwe na kada maarufu wa CCM, Kingunge Ngombale Mwiru, alisema: “Kwa sasa sina cha kusema, bwana mwandishi, no comment, ila nitatoa comment zangu wakati muafaka utakapowadia.”
Naye Mwenyekiti wa CCM, mkoa wa Singida,  Mgana Msindai, alisema kwa sasa hana maoni na kuomba apatiwe muda hadi leo.
Mbunge wa Ilala, Mussa Azan Zungu, alisema hana maoni na anasuburi chama kitoe maamuzi yake.

NIPASHE

Klabu ya soka ya Azam ya Tanzania Bara imeanza mazungumzo rasmi ya kumsajili mshambuliaji hatari wa mabingwa wa Ligi Kuu ya Kenya, Gor Mahia, Michael Olunga, na imeelezwa jana jijini Dar es Salaam kwamba wako tayari kulipa Dola za Marekani 300,000 (Sh. milioni 600) ambazo wametajiwa.
Wakurugenzi na kocha mkuu wa Kituo cha Liberty cha jijini Nairobi, Kenya, Jacob Mulee ‘Ghost’, alisema kuwa viongozi wa Azam wamemfuata rasmi kwa ajili ya kumsajili Olunga na wameonyesha nia ya kumuhitaji kwenye timu yao.
Ghost ambaye aliwahi kuipa ubingwa wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) 2008 jijini Dar es Salaam, alisema kuwa kwanza viongozi wa klabu hiyo walianzia dau la Dola za Marekani 30,000 lakini aliwaeleza kuwa kiasi hicho cha fedha ni ‘dharau’ na hakifanani na kiwango cha mchezaji huyo.
“Nimeongea na (alitaja jina la kiongozi mmoja wa juu Azam) na wameonyesha nia ya kumuhitaji kweli kweli, tutazungumza nao kabla ya Ijumaa, bodi ya Azam imeenda kujadiliana,” alisema Ghost ambaye pia aliwahi kuipeleka Harambee Stars katika fainali za Afrika (AFCON) mwaka 2004.
Aliongeza kwamba mbali na kuwa na ofa ya kwenda kufanya majaribio katika klabu ya Bidvest Wits ya Afrika Kusini, Olunga yuko mbioni kwenda Ulaya kufanya majaribio.
“Na hata akisaini Azam, mkataba wake utakuwa wazi ili akitakiwa kwa majaribio Ulaya aende. Hata ofa ya Afrika Kusini tuliisimamisha kwa ajili ya kuangalia mipango ya Ulaya kwanza, kiwango chake si cha kucheza Afrika, Ghost.
Aliongeza kwamba Olunga amebakiza miezi minne ya kuitumikia Gor Mahia ambayo anaichezea kwa mkopo akitokea Thika United ya Kenya.
Gor Mahia kwa sasa imemkataza Olunga kuzungumza na vyombo vya habari na kumtaka aelekeze nguvu na akili kwenye mashindano ya Kombe la Kagame ambapo timu yake leo itacheza mechi ya hatua ya nusu-fainali dhidi ya Al Khartoum National ya Sudan.

JAMBOLEO

Taasisi ya kupambana rushwa TAKUKURU imetangaza ukomo wa matumizi ya fedha  za kugharamia shughuli za kampeni  kwa nafasi ya Urais ni shilingi bilioni 5 tu.
Wakati huo huo TAKUKURU  imesema kuwa hivi sasa inakunjua makucha na kuwataarifu wagombea wote kutotumia njia chafu kwa ajili ya kupata madaraka.
Mkurugenzi wa TAKUKURU Edward Hosea amesema  sharia ya gharama ya uchaguzi inamtaka mgombea nafasi ya Urais kutumia bilioni 5 tu katika kampeni.
Pia sharia hiyo inamtaka mgombea  kutumia milioni 80 kwa jimbo kubwa na jimbo dogo milioni 50 na jimbo la kawaida milioni 30.
Alisema ni vyema vyama vya siasa  kuwa na akaunti maalum ili mkaguzi na mthibiti wa hesabu za Serikali  kufanya hesabu ili kuona  kiasi cha fedha zilizotumika baada ya uchaguzi kukamilika.
Dk.Hosea alisema fedha hizo ni kwa ajili ya kuendeshea kampeni hivyo wasitumie nafasi hiyo kurubuni wananchi ili wapate uongozi.

MWANANCHI

Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam kimeitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kusimamia kwa makini uandikishaji wapigakura jijini hapa ili wakazi wote wapate fursa ya kuandikishwa, ndani ya muda uliopangwa.
Katibu wa Siasa, Itikadi na Uenezi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Juma Simba aliwaambia wanahabari jana kuwa ufanisi katika uandikishaji utasaidia kumaliza idadi kubwa ya wakazi ambao bado hawajaandikishwa hadi sasa.
NEC inatakiwa kuwa makini kukamilisha uandikishaji kwa kuongeza mashine na watendaji ili wakazi wengi wa Dar es Salaam waandikishwe,” alisema.
Simba alisema CCM haitatetereka na uamuzi wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuhamia Chadema.
Alisema uamuzi huo siyo wa kwanza, kwani Augustine Mrema aliwahi kuondoka CCM na kujiunga na upinzani.
Kauli ya kiongozi huyo imekuja siku moja tangu Lowassa na mkewe, Regina, waihame CCM na kujiunga na Chadema na kuahidi kuendelea na safari ya matumaini ndani ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
“Lowassa alijiunga CCM kwa ridhaa yake, hakuna aliyemshurutisha na ametoka kwa ridhaa yake kwenda Chadema hakuna aliyemshurutisha. “CCM itabaki kuwa CCM zaidi ya hilo, lipi jipya?”
Simba alisema tishio kwamba Lowassa ataondoka na makada wengi wa chama hicho ni propaganda za kupuuzwa.
Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva alisema muda wa kuandikisha wapigakura utaongezwa baada ya kujua idadi ya watakaosalia ifikapo mwisho wa kujiandikisha Agosti 31.
“Kwa sasa hatuwezi kusema tutaongeza siku ngapi, lakini ikifika siku ya mwisho tutajua watu wangapi wamebaki na hapo ndipo tutaongeza muda au la,” Lubuva.
Alisema utaratibu wa kuanza uandikishaji kuanzia saa moja asubuhi hadi 12 jioni, unaweza kuongeza kasi ya uandikishaji na hivyo watakaosalia watapewa muda kulingana na idadi yao.
Licha ya NEC kutoa agizo kwa mawakala wa BVR kuanza kufungua vituo kuanzia saa moja asubuhi, badala ya saa mbili, baadhi ya mawakala katika vituo wamekaidi agizo hilo.
Hata hivyo, agizo hilo lilionekana kupuuzwa na mawakala wa baadhi ya vituo ambao walifungua vituo hivyo kati ya saa mbili na saa tatu asubuhi.

No comments:

Post a Comment