Vyama vitatu kufungua pazia la urais


Mwenyekiti wa Nec, Jaji Damian Lubuva (katikati) akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuhusu ratiba na utaratibu wa uchukuaji wa fomu za wagombea katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 25 mwaka huu.


Dar es Salaam. Pazia la kuchukua fomu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) za kugombea kiti cha urais katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 25 mwaka huu, linafunguliwa rasmi leo kwa wagombea wa vyama vya UPDP, TLP na DP.

Hata hivyo, ratiba iliyotolewa na NEC haikujumuisha siku ambazo mgombea wa Chadema, ambaye anawakilisha vyama vingine vitatu vya NLD, CUF na NCCR-Mageuzi, kwa kuwa havijapeleka barua kutaarifu utaratibu wao.

Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva alisema kuwa UPDP itachukua fomu hizo saa 3:00 asubuhi, ikifuatiwa na TLP saa 6:00 mchana wakati DP itafika ofisi hizo saa 8:00 mchana.
Lubuva alisema kuwa Agosti 4, itakuwa zamu ya CCM kuchukua fomu hizo na imepangiwa saa 6:00 mchana. Alisema mwisho wa kuchukua na kurudisha fomu ni Agosti 20.

Agosti 5, saa 3:00 asubuhi itakuwa zamu ya Alliance for Democratic Change (ADC) na Tadea wakati ACT- Wazalendo wakitarajiwa kuchukua fomu hizo Agosti 17.

“Baadhi ya vyama vya siasa vimesema vinakuja na wanachama wao kuchukua fomu kwa shamrashamra. Shamra shamra ziwepo, lakini zisivunje amani ya wananchi. Haki hiyo isifanywe kukatiza uhuru wa watu wengine,” alisema Lubuva.
Mwenyekiti huyo, ambaye aliambatana na Kamishna wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema wanatarajia idadi kubwa ya wanachama kusindikiza wagombea wao wakati wa kuchukua fomu, lakini ni watu wachache watakaoruhusiwa kuingia ndani ili shughuli nyingine kwenye jengo hilo zisisimame.

Lubuva alisema kuwa ni vema wagombea urais wachukue fomu hizo mapema ili waweze kuwatafuta wadhamini wasiopungua 200 katika mikoa minane ya Bara na miwili Zanzibar.
Pia, NEC iliwaonya wanasiasa wanaotoa matamshi yenye uchochezi huku akitolea mfano maneno yaliyotamkwa na kiongozi mmoja wa chama cha siasa kuwa chama chake kitashinda Uchaguzi Mkuu ujao hata kwa goli la mkono.

“Viongozi wawe makini wasitoe matamshi yanayoweza kuleta tafsiri mbaya. Goli la mkono ni matamshi yasiyo na breki,” alisema Lubuva.

Vile vile, Lubuva aliwataka wananchi kutokubali kutoa kadi zao za kupigia kura kwa ajili ya kupewa mikopo, kama ambavyo kundi moja la vijana limedaiwa kufanya katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Mkuu wa Idara ya Uendeshaji Uchaguzi, Clothilde Komba alisema kuwa wagombea wote watachukua fomu hizo bila malipo, lakini watapaswa kutoa Sh1milioni kwa mgombea wa urais, Sh50, 000 kwa kiti cha ubunge na Sh5, 000 kwa udiwani.

Akizungumzia mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu hizo, Kova alisema kuwa wagombea wa vyama vyote wanatakiwa kutumia Barabara ya Obama, kisha watawaacha wapambe wao katika eneo la Gymkhana.

No comments:

Post a Comment