Polisi mkoani hapa wamekamilisha upelelezi wa tuhuma
zinazomkabili Naibu Spika, Job Ndugai kumshambulia kwa fimbo kada
mwenzake wanayewania kuteuliwa kuwania ubunge kwa tiketi ya CCM Jimbo la
Kongwa, Dk Joseph Chilongani.
Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Dodoma, David Misime alisema jana kuwa kinachosubiriwa ni ripoti ya
daktari aliyemhudumia mgombea huyo ili kuendelea na hatua nyingine za
kisheria.
Juzi jioni wagombea wenzake wengine wa ubunge
jimbo hilo, walifika mjini hapa kwa lengo la kuzungumza na Kamanda
Misime lakini walikwama na ilipofika saa mbili usiku, walitakiwa kwenda
saa 3.00 usiku kuonana naye.
“Sisi tunashangaa mgombea
huyu aliyefanya kitendo hiki bado yuko nje kwa hiyo tumeamua kuja
kuonana na Kamanda wa mkoa ili waweze kuchukua hatua mapema,” alisema
mmoja wa wagombea hao, Simon Ngatunga.
Akizungumzia suala hilo Misime alisema walimkamata na kumhoji na aliachiwa baada ya kujidhamini mwenyewe.
Alisema
jeshi la polisi linafanya kazi zake kwa kuzingatia sheria, kanuni na
taratibu na halitamuonea mtu yeyote kutokana na fedha alizonazo au
umaarufu, bali kazi itafanyika kwa weledi mkubwa.
Dk Chilongani aliyeruhusiwa jana kutoka hospitali ya Wilaya ya Kongwa alikokuwa amelazwa alisema:
“Hali
yangu si nzuri sana kwa sababu presha si nzuri lakini kwa sababu jana
(juzi) habari zilienezwa katika mitandao kwamba nimekufa ziliwashtusha
watu na kuwafanya ndugu kumiminika kwa wingi, waliamua kuwaomba
madaktari waniruhusu ili niendelee na matibabu nyumbani,” alisema. Hata
hivyo, alisema kutokana na hali yake kutorejea katika hali ya kawaida
jana hakuweza kuhudhuria mkutano ya kujinadi uliokuwa ufanyike katika
kata mbili.
“Kama CCM wakiniambia nilete malalamiko
yangu kwa maandishi nitafanya hivyo lakini ninaomba haki itendeke,
utaratibu wa sheria utafuatwa,” alisema.
Alikanusha
maelezo ya polisi kwamba yeye ndiye aliyekwenda kutoa maelezo polisi
siku alipojeruhiwa na Ndugai... “Nilikuwa sijielewi ningewezaje kutoa
taarifa ya tukio siku hiyo? Waliotoa taarifa ni ndugu zangu.”
Ndugai
anadaiwa kumshambulia Dk Chilongani kwa kumpiga ngumi na fimbo hadi
kuzimia Jumanne iliyopita walipokuwa katika kampeni za kujinadi.
No comments:
Post a Comment